Pages

Saturday, September 7, 2013

JE, UTAMFUNIKA NUHU?




 TAZAMA
Mwanzo sura 6-9 inazungumza kuhusu mtumishi wa Mungu Nuhu ambaye Mungu alimmwamuru kutengeneza Safina ili kukisaza kizazi toka mafuriko ambayo aliyakusudia kwa wanadamu waliomwasi. Huyu ni mtumishi ambaye Mungu alimtumia kwa jinsi ya tofauti sana.

Baadaye tunaona akiwa katika udhaifu:
Mwanzo 9:20-21
Ø  Hapa mtumishi wa Mungu amelewa mvinyo hadi kuwa uchi katika hema yake.
Mwanzo 9:22-23
Ø  Ham aliona uchi wa baba yake yake akaenda kuwaambia kaka zake nje
Ø  Lakini, Shem na Japhet walichukua nguo na kumfunika baba yao; hawakumwangalia uchi wake.

TUNACHOJIFUNZA
1.   Mungu anaweza kuruhusu kuona madhaifu ya wenzetu akitaka kuona mwitikio wetu.
2.   Baadhi yetu hufurahia kutangaza udhaifu wa ndugu zao (hata wakati mwingine Baba yao –Mchungaji-) kama ilivyokuwa kwa Ham
3.   Wengi wetu tunapoona mwezetu maefanya kosa/dhambi; hufurahia na kuanza kutangaza, wakati mwingine k=hata kwa kusema, ‘Nilijua hajaokoka’  au ‘alijikuwa kimbelembele, nilijua hafiki mbali’.
4.   Watu wa Mungu (kama ilivyokuwa kwa Shem na Japhet), hutoa msaada kwani ‘upendo husitiri wingi wa dhambi’.
5.   Yesu angeangalia udhaifu wetu kwa jicho tunaloangalia udhaifu wa wenzetu, asingekuja ulimwenguni. Lakini, yesu huangalia udhaifu wetu kwa jicho la upendo ili kwa upendo huo tunabadilika. (Mithali 10:12 – ‘upendo husitiri wingi wa dhambi’)

Matokeo
Nuhu alimlaani Ham na laana hiyo ilikifuata kizazi chake cha Wakaanani. Unapohukumu/ kutangaza mudhaifu wa wenzako, roho hiyo inakufuata na itakuangamiza.

Swali Muhimu
Unaitikiaje unapomkuta mwenzako ametenda kosa? Unaposikia jambo lisilo zuri kuhusu ndugu yako, unafanya nini?
Je, utakuwa msambazaji wa maneno mabaya ukidhani ni sifa njema;
au
Utamwombea na kumshauri
Hizi ni nguvu mbili zinazofanya kazi kanisani siku hizi, moja inaishia kwenye maangamizi ya kiroho na nyingine kwenye ukombozi na kuimarisha kanisa. Uchaguzi ni wako.
Swali linabaki, Je utamfunika Nuhu? 

MAISHA MAPYA YA WOKOVU





MPANGO WA WOKOVU
1. Mungu anakupenda na ana mpango mzuri kwa maisha yako Yohana 3:16, 10:10b
2. Mwanadamu ametenda dhanbi na kutengwa na Mungu Warumi 3:23, 6:23, Waefeso 2:8-9
3. Yesu Kristo pekee ndie mwokozi wetu. Alikufa kwaajili yetu na akafufuka tupate uzima Warumi 5:8, Yohana 14:6, 1wakorintho 15:3-6
4. Lazima kumpokea Yesu kama mwokozi Yohana 1:12, Ufunuo 3:20, Warumi 10:9

KUUNGAMA DHAMBI
Si mpango wa Mungu utende dhambi. Lakini, kama wanadamu, tunakumbana na majaribu. Hii ina maana kuwa, bado tunapambana na dhambi maishani mwetu. Kinachotokea unapotenda dhambi si kupoteza wokovu wako, bali ushirka wako na Mungu uaathirika. Kama baba wa upendo, Mungu ametoa njia ya kushinda majaribu, na kumrudia tunapotenda dhambi. Biblia inasema ‘Kama tukisema hatuna dhambi twajidanganya wenyewe, na kweli haimo ndani yetu. Kama tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki, atatusamehe dhambi zetu zote na kutusafisha na uovu wetu wote’ (1Yohana 1:8-9)

Kuungama dhambi si kusema tu ‘nimefanya dhambi’. Ungamo la kweli linataka:
1.     Uwe mkweli. Tambua dhambi/kosa ulilotenda
2.     Tubu dhambi kwa Mungu (ukimaanishaa kuziacha dhambi nakutotenda dhambi tena) Zaburi 32:5
3.     Uwe wazi (mwambie Mungu hakika ulichotenda)
4.     Uwe haraka kutambua kosa lako. Mara unapogundua kuwa umetenda dhambi, ungama. Kama si hivyo upo katika hatari ya kuanguka katika dhambi nyingine zaidi.
5.     Uwe mnyenyekevu kwa kuomba msamaha kwa wote walioathioriwa na dhambi yako Yakobo 5:16, Mathayo 5: 23-24, 1Yohana 5:20
6.     Kubali msamaha. Hautakiwi kuendelea kutubia dhambi ambayo umeshatubia kana kwamba Mungu hasamehe makosa. Kama Mungu ametusamehe, ni muhimu kukubali msamaha huu, na kuamini, na kumshukuru. Kataa mashtaka ya shetani kwamga haukusamehewa/ au hauwezi kusamehewa.

KAMA UMEOKOKA JUA SASA WEWE:-
1.     Ni kiumbe kipya (2Wakorintho 5:17)
2.     Ni mwana wa Mungu (Yohana 1:12, Warumi 8:14-15, Wagalatia 3:26, 4:6)
3.     Umekombolewa na kusamehewa dhambi zako zote (Wakolosai 1:14)
4.     Umewekwa huru kabisa, mbali na hukumu na nguvu ya dhambi ( Warumi 8:1; 6:1-6)
5.     Unayo haki bila aibu kukisogelea kiti cha enzi cha Mungu kuomba neema nyakati za mahitaji (Waebrania 4:16)
6.     Una haki katika Kristo, umesamehewa dhambi zote (Warumi 5:1)
7.     Ni mtumwa wa haki (Warumi 6:18)
8.     Ni mtakatifu (Waefeso 1:1, Wakorintho 1:2, Wafilipi 1:1)
9.     Ni chumvi na nuru ya ulimwengu (Mathayo 5:13-14)
10.  Ni rafiki na chaguo la Yesu Kristo kumzalia matunda (Yohana 15:15-16)
11.  Ni mtumishi wa mungu (Warumi 6:22, Waefeso 3:1; 4:1)
12.  Ni hekalu takatifu, mahali ambapo Mungu Roho Mtakatifu anakaa (1Wakorintho 3:16,; 6:19)
13.  Umenunuliwa kwa gharama kubwa, Damu ya Yesu, na hivyo ni mali ya Mungu, unaishi kwaajili ya Kristo (1Wakorintho 6:19-20, 2Wakorintho 5:14-15)
14.  Ni kiungo katika mwili wa Kristo (1Wakorintho 12:27, Waefeso 5:30)
15.  Umepatanishwa na Mungu kwa njia ya Yesu, hivyo ni mpatanishi (2Wakorintho 5:18-19)
16.  Ulisulubiwa pamoja na Kristo, si wewei unayeishi, ni Kristo ndani yako (Wagalatia 2:20)
17.  Ulichaguliwa na Kristo kabla ya kuwekwa misiingi ya ulimwengu kuwa mtakatifu bila ya mawaa mbele zake (Waefeso 1:4)
18.  Ni mrithi katika ufalme wa Mungu, kwa sababu ni mtoto wake (Wagalatia 4:6-7)
19.  Ni mtendakazi wa Mungu, uliyezaliwa mara ya pili (uliyeokoka) ili kufanya kazi yake (Waefeso 2:10)
20.  Ni mtakarifu na mwenye haki wa Mungu (Waefeso 4:24)
21.  Ni raia wa mbinguni (Wafilipi 3:20, Waefeso 2:6)
22.  Ni msafiri katika dunia hii, ambayo unishi kwa muda tu (1Petro 2:11)
23.  Ni aliyekombolewa toka utawala wa shtani na kupelekwa kwenye ufalme wa mungu (Wakolosai 1:13)
24.  Ni adui wa shetani (1Petro5:8)
25.  Ni mzaliwa wa Mungu. Shetani hana mamlaka kukukugusa (1Yohana 5:18; Kristo mwenyewe anaishi ndani yako (Wakolosai 1:13)
26.  Umezaliwa na Mungu, mtakatifu na mpendwa (Wakolosai 3:12; Wathesalonike 1:4)
27.  Umepewa ahadi kuwa mno toka kwa Mungu (2Petro 1:4)
28.  Utakua kama Kristo atakaporudi mara ya pili (1Yohana 3:1-2)
29.  Kwa neema ya Mungu upo kama hivyo ulivyo (1Wakorintho 15:10)

JINSI YA KUTEMBEA NA YESU
1.     Soma Biblia kila siku ili umjue yesu vema
2.     Zungumza na Mungu kila siku kwa njia ya maombi
3.     Ruhusu Mungu atawale maisha yako, ukijitoa kwa mapenzi yake
4.     Zungumza na wengine kuhusu yesu
5.     Shirikiana na wengine katika ushirika/ibada mahali Yesu anahubiriwa
6.     Jiunge na mshirika mmoja au wawili ambao mnaweza kuomba pamoja na kushirikiana mafanikio na matatizo yako
7.     Onyesha maisha yako mapya kupitia upendo na kuwajali wengine

JINSI YA KUISHI MAISHA YA WOKOVU KILA SIKU
1. Andaa moyo wako: Jichunguze, Ungama dhambi, Omba ufahamu Zaburi 5:3; 139:23-24; 51:10, Waebrania 4:16
2. Jifunze biblia. Kila unaposoba Biblia andika neno lililokusa sana, wazo kuu na maana ya neno katika maisha yako. Jiulize kama kuna amri au mfano wa kufuata, dhambi ya kutubia na ahadi ya Mungu kwako
3. Omba: Ongea na Mungu kuhusu neno ulilosona, mwabudu na kumsifuMungu kwa ukuu wake, na mpe Mungu mahitaji yako
4. Mwimbie Mungu wimbo wa sifa au tenzi. Wimbo wa kuabudu,  wa taratibu na muziki mwororo utasaidia kukusogeza karibu na Mungu na kumsifu Yeye
5. Omba kujazwa na Roho Mtakatifu. Omba maombi ya kujitoa mbele za Mungu, mfano; ‘Baba katika Jina la Yesu,        
Najitoa mbele zako,
Niwe chombo kikufaacho,
Tawala akili zangu na kila ninachofikiri,
Tawala macho yangu na kila ninachotazama,
Tawala masikio yangu na kila ninachosikia,
Tawala ulimi wangu na kila ninachonena,
Tawala moyo wangu na tabia zangu,
Tawala mikono yangu na yote nifanyayo,            
Tawala miguu yangu na pote niendapo,
Tawala mwili wangu ni hekalu lako Bwana,
 Nijaze na Roho Mtakatifu,
 Nataka kukutii, Nataka kukufuata wewe
Siku zote za maisha yangu, Nisaidie Bwana, Haleluya! Sante Yesu!

6. Fanyia kazi yale uliyojifunza
7. Kariri mstari mmoja, uandike katika daftari.

KARIBU KTK MAISHA MAPYA

MPANGO WA MUNGU KUKUFANIKISHA KIUCHUMI



UTANGULIZI
Mpango wa Mungu kwa mwanadamu ni wa ajabu sana, haufungwi na muda au mahali ambao ukifuatwa kwa uaiminifu na ukamilifu, utimilifu wake si wa mashaka hata kidogo. Hata hivyo, Mungu angependa ushiriki katika mafanikio yako ili uwe sehemu ya mafanikio yako kama ilivyokuwa katika Yohana 11:39, ambapo Yesu aliwataka ndugu wa Lazaro (aliyekufa), washiriki katika muujiza wa kufufuka kwa Lazaro kwa kuliondoa jiwe

UTII
Ili Mungu amwage baraka juu ya maisha yako, unahitaji kuwa mtii kwa Neno lake (Kumb 28:2). Kwa hakika, kutii Neno la Mungu ni muhimu katika mafanikio yako kiuchumi (Yoshua 1:8)

Mafanikio ya maisha yako ya mbele kiuchumi yana uhusiano wa moja kwa moja na jinsi unavyotii kanuni za Mungu kuhusu utoaji. Unahitaji kushiriki katika muujiza wako, Neno la Mungu linaagiza kumheshimu BWANA kwa mali zetu ili tupate mavuno mengi maishani (Mithali 3:9-10).

AHADI
Mungu anataka kukubariki katika kila eneo la maisha yako, ikiwa ni pamoja na hali yako ya uchumi. Kumbuka tunaposema uchumi ni fedha na mali nyingine kama mifugo, mashamba,n.k. Hivyo, Mungu anapenda upate fedha na mali ili uvitumie kwa utukufua wake.
1.    Hakuna kizuizi chochote cha baraka za Mungu kwa sababu vyote ni mali yake na haviwezi kuisha kwani yeye ndiye aliyeviweka (Wafilipi 4:19)
2.    Baraka za Mungu zitaendelea kukufuata wewe na watoto wako (Zaburi 115:14).
3.    Mungu atakufundisha jinsi ya kufanikiwa (Isaya 48:17).
4.    Mungu atabariki kazi za mikono yako (Kumb. 28:12)
5.    Mungu atakuwezesha kufanikiwa (Kumb 8:18)
6.    Kwa jinsi unavyozidi kumtafuta, Mungu atakutana na mahitaji yako (Zaburi 24:10)
7.    Ikiwa utamtii na kumheshimu, Mungu atakubariki wewe na jamaa yako (Zaburi 112:1-3)
8.    Baraka za Mungu kwako ni njema wakati wote (Mithali 10:22)
9.    Mungu ataubariki uaminifu wako (Mithali 28:20)
10. Unapowapa wahitaji, Mungu naye atakutana na mahitaji yako; Hautapungukiwa kamwe (Mithali 28:27)
11. Ukitoa kwa moyo mkunjufu, Mungu atakumwagia baraka tele (2Wakorintho 9:6-7)
12. Unaweza kufungulia baraka za Mungu maishani mwako leo iwapo utamtii Mungu katika maeneo ya utoaji. Baraka katika utoaji ni mfano wa kupanda mbegu. Biblia inasema kila mtu apandacho ndicho atakachovuna (Wagalatia 6:7). Ukitoa kitu/vitu dhaifu tegemea kupokea kidogo. Angalia mfano wa Kaini na Habili (Mwanzo sura ya Nne).

Sijaona mkulima ambaye anapanda bila ya kutegemea kuvuna. Pia wakati wa mavuno, mkulima mwenye busara huweka mbegu/hupanda mbegu kwaajili ya mvuno mengine, wakati ziada ikitumiwa kukidhi mahitaji yake binafsi. Hii ndio kanuni ya mafanikio, na Mungu ameahidi katika hili (Luka 6:38)

UNACHOHITAJI NI MBEGU
Wakati Mungu ndiye atoaye mavuno, mimi na wewe tunahitaji kupanda mbegu. Huu ni wajibu wetu.

Kanuni Saba Za Mavuno
1. Lazima mbegu ipandwe ili kutoa mavuno (Yohana 12:24). Mbegu inayozaa lazima kwanza ipandwe, hata kama mbegu inaweza kuonekana ndogo mikononi mwa mkulima, lakini unapoipanda unakua umeachilia uwezo wake wa kuzaa mtunda mengi.
2. Mbegu lazima ihuishwe (Yohana 12:24) Mavuno yaliomo ndani ya mbegu yamefichwa hadi mbegu ihuishwe.. Wakati mbegu ikiwa imehuishwa huonekana haifai kwa matumizi yoyote. Baada ya muda huu ndipo mbegu inaota na kukua tayari kwa mavuno. Kumbuka unapopanda mbegu katika kazi ya Mungu, inakua haifai kwa matumizi yako binafsi, lakini inahifadhiwa na kuzidishwa. Baada ya kuzidishwa inarudi kwako kwaajili ya mavuno.
3. Panda kile unachotegemea kuvuna (Mwanzo 1:12) Ukipanda maharage hauwezi kuvuna mpunga, vivyo hivyo kwa kila mbegu upandayo. Kwa kuzingatia kanuni ya kupanda na kuvuna, utavuna mazao ya aina ya mbegu uliyopanda.
4. Kiasi cha mavuno kinategemea kiasi cha mbegu ulizopanda (2Wakorintho 9:6). Mungu hawezi kukupangia kiasi utakachovuna, wewe mwenyewe unahitaji kukipanga kwa kujua kiasi kipi upande na uvune kiasi gani. Mkulima apandaye heka tano (5) za mpunga atapata mavuno zaidi kuliko aliyepanda nusu heka (0.5).
5. Panda kwenye udongo mzuri, wenye unyevu (Mathayo 13:3,8). Mbegu lazima ipandwe kwenye udongo mzuri ili iote na kutoa mvuno mazuri.. udogo mzuri ni wenye rutuba, ulioandaliwa vizuri, wenye kasi cha maji cha kutosha tayari kupokea mbegu.
6. Mavuno huja baada ya kusubiri kwa muda (Marko 4:26-2) Inachukua muda kupanda mbegu, kuota, kukua hadi kufikia mavuno. Nguvu ya mavuno inatokea taratibu jinsi mmea unapokua, na wakati fulani unaweza kuona kuwa mazao yangu yatatoa mavuno mengi.
7. Lazima shamba litunzwe ili kutoa mavuno (Mathayo 13:3,7) Mbegu iliyopandwa lazima itunzwe vizuri ili kutoa mavuno. Inahitaji maji ya kutosha, magugu yatolewe, palizi lifanyike kwa wakati ili kuruhusu mbegu kukua kwa afya njema na itoe mavuno mengi na mazuri.

Unapopanda mbegu katika Bwana, unapanda kwa imani na kuondoa magugu kwa njia ya maombi na kumsifu Mungu.

KUMBUKA
1. Usile mbegu Watu wengine wenye mahitaji wamesahau na kufanya makosa kwa kula mbegu badala ya kupanda. Ni mbegu iliyopanwa pekee ndiyo inweza kuzaa mavuno mengi
2. Endelea kupanda mbegu Usiache kupanda mbegu ili kupata mavuno mengi (Mhubiri 11:6)

HITIMISHO
Kupanda ni kanuni ya mbinguni, kanuni iliyowekwa na Muumbaji Mwenyewe. Kama mkulima yeyoye anavyopanda mbegu ardhini akitarajia mavuno, kwa hiyo kanuni hii itamsaidia yeyote anayetaka kufanikiwa kiuchumi kama ataitumia kwa uaminifu. Ni rahisi, panda mbegu, vuna mavuno. Kumbuka, siri ya mavuno yako ipo katika mbegu.

MBEGU NI NINI?
Matoleo ya aina yoyote kama vile:
Sadaka,                          Kikumi,                 Uaminifu, Kuwaona wenye shida,
Kusaidia wenye shida,     Kutmbelea wahitaji,        Kuwapenda wengine n.k

PANDA MBEGU LEO